:: Home :: About Us :: NGO Profiles :: NGO Board :: Site Map :: Feedback :: Contact Us   :: NGOs MIS  
      KEY AREAS
Youth Empowerment  
Agriculture  
Capacity Building  
Economic Empowerment  
Education  
Environment  
Good Governance  
Health  
HIV/AIDS  
ICT  
Legal Rights  
Multi Sectors  
People with desability  
Poverty Alleviation  
Service Sector  
 
  USEFUL LINKS
a
Fanya Malipo ya Ada za NGOs
a
President's Official Website
a
National Council of Ngo's
Ministry of Community Development,Gender and Children
Tanzania National Website
Community Development Insititutes
Tanzania Development Gateway
United Republic of Tanzania, Wananchi Portal
  More Links >>

 

 

 

KAZI ZA IDARA YA URATIBU WA NGOs

1.0   UTANGULIZI

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto inalo jukumu la kuratibu, kufuatilia na kusimamia utekelezaji wa shughuli za NGOs nchini.  Kimsingi kazi hii inatekelezwa kupitia Idara ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo Kiserikali (NGOs Coordination Department). Kulingana na muundo wa Wizara, Idara hii ina sehemu kuu mbili, ambazo ni Uratibu na Ufuatiliaji (Coordination and Monitoring) na Usajili wa NGOs (Registration).

 Katika kutekeleza jukumu hili Idara  imejiwekea dira ambayo inaiongoza ili kufikia dira ya Wizara na hatimaye dira ya Taifa. Dira (Vision) ya idara  ni “Kuwa na mazingira bora yatakayowezesha sekta ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kufanya kazi kwa ubunifu, ufanisi, na mashirikiano endelevu na Serikali na wadau hivyo kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya jamii na ya kiuchumi. Katika harakati ya kufikia dira ya Idara, aidha tunayo Dhamira (Mission) ambayo ni “Kusimamia, na kuwezesha Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kutekeleza majukumu yao kikamilifu kama yalivyoainishwa katika katiba zao kwa maendeleo ya jamii na ya kiuchumi nchini”.

Ili kutekeleza jukumu hili kikamilifu tunazo nyenzo kuu mbili ambazo ni Sera ya Taifa ya NGOs (2001) na Sheria ya NGOs Na. 24/2002. Nyenzo hizi zote zimeainisha na kusimika rasmi vyombo vikuu viwili vya kitaifa ambavyo ni Bodi ya Taifa ya Uratibu wa NGOs (National NGOs Coordination Board) na Baraza la Taifa la NGOs (National council for Non-Governmental Organizations). Vyombo hivi viwili ni muhimili mkubwa katika usimamizi, uratibu, utetezi na ushawishi wa NGOs kufanya kazi kwa uadilifu na uwajibikaji na vimeundwa kisheria.

 Bodi ya Taifa ya Uratibu wa NGOs imeanzishwa kwa Kifungu cha 6(1) cha Sheria ya NGOs Na. 24 ya mwaka 2002 na Baraza la Taifa la NGOs Kifungu cha 25 (1) cha sheria hiyo hiyo. Ili kurahisisha utekelezaji, uratibu na ufuatiliaji wa shughuli za NGOs tumeanzisha utaratibu wa usajili wa NGOs katika ngazi ya Taifa, Mkoa na Wilaya. Aidha, tuliteua wasajili Wasaidizi ambao ni Maafisa Mipango katika ngazi ya mkoa na Makatibu Tawala katika ngazi ya Wilaya. Kutokana na idara kuwa chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, imeonekana kuwa ni vyema Maafisa Maendeleo ya Jamii katika ngazi za wilaya na mikoa kutumika kama Wasajili wasaidizi katika ngazi hizo. Hata hivyo, mchakato wa uteuzi wao haujakamilika ila unaendelea vyema. Aidha, elimu stahiki juu ya wajibu wao kama wasajili wasaidizi walishapatiwa. Pamoja na ufuatiliaji NGOs kwa mujibu wa Sheria ya NGOs Na. 24/2002 wanatakiwa kuleta kwa Msajili wa NGOs Makao Makuu taarifa zao za kazi za kila mwaka na taarifa za fedha zilizokaguliwa za kila mwaka. Hivyo, taarifa inayopatikana wakati wa ufuatiliaji na taarifa zao za mwaka zinahakikiwa ili kupata hali halisi ya utendaji kazi wao katika maeneo husika.

2.0   USAJILI NA UFUATILIAJI WA UTENDAJI KAZI WA NGOs NCHINI

Baada ya kupitishwa kwa Sheria ya NGOs Na. 24 ya mwaka 2002, Idara ilipata mamlaka na uwezo kamili wa kusajili, kusimamia, kuratibu na kufuatilia utendaji wa NGOs katika ngazi mbalimbali. Jukumu la usajili ambalo kisheria ni jukumu la Bodi ya Taifa ya Uratibu wa NGOs lilikasimiwa rasmi kwa Msajili  wa NGOs (Registrar of NGOs) ambaye ni Katibu wa Bodi ya Taifa ya Uratibu wa NGOs na Mkurugenzi  wa Idara. Kimsingi utekelezaji wa Sheria hii katika maana ya kusajili NGOs chini ya sheria hii ulianza rasmi mwezi Januari, 2005.

3.0   UTOAJI TAARIFA ZA KAZI NA ZA FEDHA ZA NGOs

Kwa mujibu wa Sheria ya NGOs Na. 24/2002 Kifungu 29 (1) (a-b) kinayataka Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yaliyosajili chini ya Sheriahii kuandaa na kuleta taarifa zao za kazi za mwaka na taarifa za mapato na matumizi ya fedha zilizohakikiwa na Mkaguzi wa Mahesabu. Idara imekuwa ikipokea taarifa hizi kutoka kwa mashirika yaliyosajili na yale yaliyopewa vyeti vya ukubalifu. Mapitio ya taarifa hizi yameonyesha kuwa zimekuwa zikianisha shughuli mbalimbali zilizotekelezwa kwa mwaka kwa kuzingatia sekta ya kipaumbele, malengo, mafanikio na changamoto zinazowakabili. Kwa ujumla changamoto zinazowakabili ni ukosefu wa fedha za kutosha kuendesha shughuli zao, ukosefu wa ujuzi katika nyanja za kiuendeshaji na utawala, kukosa stadi za ubunifu na hivyo kuendelea kuwa tegemezi kwa wafadhili, usiri wa baadhi ya NGOs ambazo tayari wamepata wafadhili na kutokuwa wazi katika utendaji kazi wao.  Kiutendaji taarifa hizi zimewezesha Idara kutambua uhai wa mashirika haya, kiwango cha fedha ambacho kilipatikana na kutumika kwa mwaka husika, kujua idadi ya wafanyakazi wageni na wenyeji/wazawa wanaofanya kazi katika Mashirika  hayo.

4.0   MATATIZO/CHANGAMOTO ZINAZOIKABILI SEKTA YA NGOs

Sekta ya NGOs nchini inakua kwa kasi sana, kwani kumekuwa na muamko mkubwa ndani ya jamiii wa kuanzisha Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ili kuweza kupambana na matatizo mbalimbali yanayoikabili jamii ya watanzania. Changamoto kubwa zinazoikabili sekta ya NGOs ni  kama ifuatavyo:-

4.1 MAHITAJI MAKUBWA YA RASILIMALI

Ukuaji huu unaenda sambamba na ongezeko la mahitaji ya rasilimali ili kuweza kutekeleza shughuli zilizokusudiwa na mashirika haya. Ongezeko hili la mahitaji ya rasilimali limekuwa ni kikwazo kikubwa kwa sekta ya NGOs kufanya kazi zake kwa ufanisi, kwani mashirika mengi ya ndani ( Local NGOs) hayana uwezo wa kupata rasimali hizo ili kuweza kutekeleza majukumu yake. Hii inachangiwa sana na kuwa na mtizamo wa wafadhili badala ya kubuni mbinu mbadala ya kupata mtaji wa kuendesha shughuli zao humu humu nchini. Hii imesababisha kuwa na utitiri wa NGOs kushughulikia agenda moja au kujikita kwenye sekta moja ambayo inapata fedha za wafadhili, kama vile UKIMWI, Mazingira, haki za binadamu, n.k.

4.2 UWEZO MDOGO WA UTENDAJI

Kuongezeka kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali hakuendi sambamba na uwezo wa Mashirika hayo kutoa huduma stahili kwa jamii husika kisekta. Wananchi wengi wamekuwa wakianzisha Mashirika yanayolenga sekta fulani ya jamii kama vile UKIMWI, Mazingira n.k huku wakiwa hawana elimu sahihi,ujuzi na ujasiriamali kuhusiana na Sekta husika. Hii imepelekea na kuwa NGOs nyingi wababaishaji ambao mara nyingi huwa ni kama bendera hufuata upepo – wakisikia kuwa sasa wafadhili wanasaidia sekta au eneo fulani basi hujikita huko ili mradi wapate fedha. Ingawa kwa sasa kunamatumaini mazuri kufuatia kutungwa na kutangazwa rasmi kwa Kanuni za Maadili ya NGOs na Baraza la Taifa la NGOs.

 4.3 UWAZI NA UWAJIBIKAJI (BRIEFCASE NGOs)

Suala la uwazi ni msingi muhimu sana katika utekelezaji wa majukumu ya Sekta ya NGOs. Uwazi kwa maana ya kuweka bayana majukumu ya Asasi husika na huduma zitolewazo na Asasi. Utelekezaji wa shughuli za Asasi husika ni lazima ziwe wazi kwa walengwa na ziwe zinakidhi mahitaji ya walengwa. Mashirika mengi yamekuwa yakianzishwa kwa manufaa ya wanachama huku wakiwatumia walengwa kama vile yatima, waathirika wa UKIMWI kama chombo kwa ajili ya kupata fedha kutoka kwa Wahisani. Fedha hizo zinapopatikana mara nyingi zimekuwa haziwafikii walengwa kutokana na kutokuwepo uwazi wa Shirika kiutendaji na ushiriki mdogo wa wanachama na walengwa wa Shirika katika maamuzi ya matumizi ya rasilimali za Shirika. Aidha suala la uwajibikaji ni msingi mkuu katia kufanikisha lengo la sekta ya NGOs nchini. Kulingana na Sheria ya NGOs, Shirika Lisilo la Kiserikali linatakiwa kutoa taarifa ya mwaka ya utekelezaji wa shughuli za Shirika ikiambatanisha na taarifa ya matumizi ya fedha. Hii inasaidia kuongeza ufanisi katika utendaji wa Shirika hivyo kuongeza uwazi wa Mashirika kwa wahisani, Serikali, Jamii na wadau wengine kwa ujumla.

4.4 MATAKWA YA WAFADHILI

Shirika Lisilo la Kiserikali huanzishwa kwa hiari na wananchi kwa kutambua tatizo au matatizo yanayoizunguka jamii husika. Hivyo basi mengi huwa na malengo yao ya awali ambayo yanalenga kutatua matatizo yaliyokwisha bainishwa. Kwauzoefu wa Mashirika yetu ya Kitanzania, mengi yamekuwa yakifanya shughuli kulingana na matakwa ya wafadhili hivyo kushindwa kutimiza lengo kuu la kuanzishwa kwa Shirika husika. Aidha, mashirika mengi yamekuwa yakianzishwa kwa kuangalia vipaumbele vya ufadhili ambavyo vingi vinakuwa havilingani na mahitaji halisi ya lengo husika. Hii imechangia kwa kiasi kikubwa kutokuonekana kwa mchango halisi wa NGOs nchini kwani mashirika mengi yamekuwa yakichangia kutatua matatizo ya aina moja bila kujali mahitaji halisi ya wananchi. Aidha, wafadhili hutumia mashirika haya kutekeleza agenda zao za siri kwani kunakuwa na mawasiliano ya moja kwa moja kati ya wafadhili na NGOs bila hata Serikali kuhusishwa. 

4.5 KUTANDAA (NETWORKING)

Mashirika mengi yasiyo ya Kiserikali yamekuwa yakifanya kazi zake katika eneo moja hasa maeneo ya mijini, hivyo kutotandaa katika sehemu nyingine, na kufanya huduma zitolewazo kutowafikia walengwa halisi. Aidha, mashirika mengi yamekuwa yakifanya kazi katika sekta nyingi kwa wakati mmoja kama vile shirika moja linajihusisha na UKIMWI, Mazingira, Elimu, yatima n.k. Hii imechangia kwa kiasi kikubwa ufanisi mdogo wa Mashirika haya, kwani si rahisi kwa shirika kama hili kuwa na utaalamu wa kutosheleza katika nyanja zote hizi. Hali kadhalika kujihusisha kwa shirika moja katika nyanja nyingi kimekuwa kikwazo kwa Mashirika ya Tanzania kukosa fedha za wafadhili kwani hupunguza uaminifu.

5.0  MATATIZO / CHANGAMOTO ZINAZOIKABILI IDARA YA NGOs

5.1 KASI KUBWA YA USAJILI

Kutokana na mwamko mkubwa walionao Wananchi wa kuanzisha Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, hasa baada ya kuwepo utaratibu mpya wa usajili chini ya Sheria ya NGOs, maombi ya usajili yameongezeka hivyo kufanya kazi ya usajili kuwa ngumu - kwa mfano kwa kila mwezi jumla ya NGOs 52 husajiliwa. Hii ni idadi kubwa ikilinganishwa na uwezo wa idara kuweza kuzifuatilia kutokana na ufinyu wa bajeti na watumishi. Kimuundo Idara inatakiwa kuwa na watumishi 27 hata hivyo waliopo sasa ni watumishi 12 hivyo bado kuna nakisi ya watumishi 8. 

5.2 UFINYU WA BAJETI  

Kama ilivyoainishwa katika majukumu ya Idara ya Uratibu wa NGOs, mengi ya majukumu yake yanahitaji fedha za kutosha ili kuweza kutekelezwa. Kazi za ufuatiliaji wa NGOs zilizotandaa nchini nzima haziwezi kufanyika kikamilifu endapo kutakuwa na ufinyu wa bajeti kama ilivyo sasa. Mathalani Katika kipindi cha mwaka 2005/2006 Idara ya NGOs ilipangiwa bajeti ya Shs. Milioni miamoja tu, hivyo kusababisha idara kushindwa kutekeleza majukumu yake kwa kiwango kinachohitajika kutokana na ufinyu wa bajeti ya Serikali. Aidha, Idara ni Sekretariati ya Bodi ya Taifa ya Uratibu wa NGOs ambayo uendeshaji wake unategemea sana bajeti ya Serikali. Kimsingi ili Bodi iweze kufanya kazi zake kwa ufanisi inahitaji angalu kuwa na bajeti ya Shs. 436,000,000/= kwa mwaka pamoja na magari 2 kuwawezesha kutembelea na kufanya kaguzi kuhusu shughuli za NGOs nchini.  

5.3 UPUNGUFU WA VITENDEA KAZI 

Kazi kubwa ya Idara ni uratibu na ufuatiliaji wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali mikoani na wilayani. Hii ni pamoja na kuzitembelea NGOs na kufanya tathmini ya utekelezaji wa majkumu yao kama yalivyoainishwa katika katiba zao, kutoa weledi kuhusu utekelezaji wa Sheria ya NGOs na kupima matokeo hasa kutambua ni kwa kiasi gani shughuli zao zimesaidia kuwaondolea wananchi matatizo yao, kuwaongezea kipato, kuchangia Pato la Taifa na kuondoa au kupunguza kero za wananchi. Kazi hii inafanywa kwa ushirikiano na Bodi ya Taifa ya Uratibu wa NGOs hivyo kuwa na haja ya kuwa na magari angalau 2 kuhudumia Bodi na Idara.  

5.4 UPUNGUFU WA WAFANYAKAZI 

Kasi ya ongezeko la usajili wa NGOs ni vyema iende sambamba na idadi au ongezeko la wafanyakazi ili kutoa huduma bora zilizosheheni ufanisi wa hali ya juu. Kwa mfano Idara haina kabisa Afisa Masijala,. Hali hii inawalazimu watumishi wachache tulionao kufanya kazi zote ili kuhakikisha kwamba wananchi wanapata huduma inayostahili hata ikibidi kuendelea na kazi baada ya saa za kazi.  

5.5 USAJILI KATIKA SHERIA MBALIMBALI 

Kama ilivyoelezwa awali kabla ya Sheria ya NGOs Na. 24/2002 usajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ulifanyika chini ya Sheria ya Vyama, Sura 337, Sheria ya Udhamini, Sura 375 na Sheria ya Makampuni, Sura 212/213. Baada ya kuanza utekelezaji wa Sheria ya NGOs hasa usajili imekuwa ni changamoto kwa Wasajili wengine na wadau kwa ujumla. Kwa mfano, imekuwa ni tatizo kubwa kwa wadau kuelewa mantiki ya kupata cheti cha ukubalifu chini ya Sheria ya NGOs na wakati huo kuendelea kulipa ada ya mwaka kwa wasajili wa awali kwani Sheria ya NGOs iko kimya katika eneo hilo. Hii imeongeza mzigo kwao kwani wanatakiwa kutumikia wasajili zaidi ya mmoja. Kama takwimu zinavyoonyesha kwenye Jedwali Na. 1 jumla ya mashirika 256 tu ndiyo yaliyoomba na kupewa Cheti cha Ukubalifu wakati inaaminika kuwa yapo zaidi ya mashirika 4,000 yaliyosajiliwa chini ya sheria nyingine kabla ya mwaka 2002. Kuwepo kwa sheria hizi na kuendelea kuwepo kwa nafasi ya usajili katika sheria hizo bila kufuta vipengele vinavyoruhusu usajili wa vyama vinavyofanya kazi kama NGOs kumefanya suala la uratibu kuwa mgumu, kutoa mkanganyiko kwa wadau wa sekta ya NGOs na kuendeleza mianya ya NGOs zisizowaaminifu kutumia fursa hii kwa manufaa yao binafsi. 

6.0 MKAKATI WA KUBORESHA

Kwa kuzingatia mafanikio na changamoto zinazoikabili Idara pamoja na sekta ya NGOs kwa ujumla, Idara imejiwekea malengo yafuatayo:- 

(i) Kufanya tafiti kuhusu fursa na changamoto zinazoikabili Sekta ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ili kuiwezesha kufikia malengo yaliyoainishwa katika MKUKUTA na hatimaye Dira ya Taifa ya 2025.

(ii) Kuanzisha Tovuti Maalum ambayo itatumika kuingiza Taarifa za Kazi na Taarifa za Fedha za mwaka za NGOs. Tovuti hii imekuwa na mfumo maalum kwa wananchi kutoa taarifa ya utendaji wa NGOs katika ngazi yoyote (Web Based Information System). Utaratibu huu unasaidia kupunguza mianya ya NGOs za Mifukoni, unaimarisha Benki ya Takwimu na kutoa fursa kwa wananchi kupata taarifa hizo kwa wadau wengi kiurahisi.

(iii) Kutoa mafunzo maalum kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii na kuwateua rasmi kuwa Wasajili Wasaidizi ili kuweza kutoa huduma bora kwa sekta ya NGOs. Mafunzo haya yameshafanyika Maafisa Maendeleo ya Jamii kufanya kazi hii ya kuwezesha usajili na kufuatilia utendaji kazi wa NGOs katika ngazi ya Mkoa na Wilaya. Hata hivyo, mchakato wa uteuzi wao bado unashughulikiwa.

(iv) Kuijengea uwezo Bodi ya Taifa ya Uratibu wa NGOs kwa kutoa fursa ya kuielewa vema Sheria ya NGOs, Sera ya Taifa ya NGOs, kufanya safari za mafunzo nje na kupatiwa vitendea kazi ili waweze kutimiza majukumu yao.

7.0 HITIMISHO 

Mafanikio ya mikakati yote tuliyojiwekea yataweza kufanikiwa kwa kiwango tarajiwa iwapo changamoto zinazoikabili idara zitashughulikiwa. Mikakati yote inalenga katika kuboresha sekta ya NGOs katika kutoa huduma bora kwa jamii.  

 

 
     
  For further information please send us a feedback or query
 
     
     
  :: Home :: About Us :: NGO Profiles :: Site Map :: Feedback :: Contact Us