:: Home :: About Us :: NGO Profiles :: NGO Board :: Site Map :: Feedback :: Contact Us   :: NGOs MIS  
      KEY AREAS
Youth Empowerment  
Agriculture  
Capacity Building  
Economic Empowerment  
Education  
Environment  
Good Governance  
Health  
HIV/AIDS  
ICT  
Legal Rights  
Multi Sectors  
People with desability  
Poverty Alleviation  
Service Sector  
 
  USEFUL LINKS
a
Fanya Malipo ya Ada za NGOs
a
President's Official Website
a
National Council of Ngo's
Ministry of Community Development,Gender and Children
Tanzania National Website
Community Development Insititutes
Tanzania Development Gateway
United Republic of Tanzania, Wananchi Portal
  More Links >>

 

 
  MASWALI, MAONI NA MAJIBU WAKATI WA MIKUTANO KATI YA BODI YA TAIFA YA URATIBU WA NGOs NA WADAU WA SEK  
  POSTED ON:  
     
  Swali 1: Bodi inafanya nini kuhusu NGOs za mfukoni? Jibu: Suala la NGOs za mifukoni si rahisi kama linavyotamkika, maana haliko wazi kama wadau wanavyofikiri. Jitihada za pamoja zinahitajika kati ya Bodi na wadau katika kubainisha ni NGOs zipi za mifukoni, ziko wapi na zinafanya nini. Katika jitihada za kulitafutia ufumbuzi suala hilo, Baraza la Taifa la NGOs limeandaa Kanuni za Maadili ya NGOs na zimeanza kutumika. Kanuni hizi zitasaidia kuzibaini na kudhibiti NGOs za mifukoni na zile ambazo hazitekelezi majukumu yake ipasavyo. Bodi iko tayari kushirikiana na wadau ili NGOs za mifukoni zichukuliwe hatua za kisheria kuliko kuendelea kuharibu taswira ya sekta ya NGO nchini. Swali 2: Je, Ni NGOs ngapi za mfukoni zimefutwa? Jibu: Hadi sasa hakuna NGO ya mfukoni iliyofutwa maana bado kuna changamoto kubwa ya kuzibainisha ni zipi, ziko wapi na zinafanya nini. Aidha, NGOs ambazo zimesajiliwa zinatambulika ziko wapi na zinafanya nini. Hata hivyo Serikali inaamini katika wadau wa sekta hii kujidhibiti wenyewe kupitia chombo chao cha kitaifa. Tunaamini kupitia Kanuni za Maadili ya NGOs ambazo zimeanza kutumika na kusimamiwa na Baraza la Taifa la NGOs basi NGOs za mfukoni zitabainika na kuchukuliwa hatua za kisheria. Swali 3: Je, Tathimini na ufuatiliaji wa utendaji wa shughuli za NGOs inafanyikaje? Jibu: Tathmini na ufuatiliaji wa utendaji kazi wa NGOs unafanywa na Bodi kupitia wajumbe wenyewe wakati wa vikao na ziara za ufuatiliaji mikoani na wilayani. Aidha, Wasajili Wasaidizi katika ngazi ya Mkoa na Wilaya wanalo jukumu pia la kufuatilia utendaji kazi wa NGOs katika maeneo yao. Katika mkakati wa kuboresha ufuatiliaji wa shughuli za NGOs nchini, Tovuti ya NGOs (www.tnnc.go.tz) iliyozinduliwa mapema Mwezi Julai, 2009 tayari baadhi ya taarifa za kazi, mapato na matumizi ya fedha ya NGOs yameingizwa ili kuongeza uwazi na uwajibikaji. Tunaamini pia kupitia Tovuti hii wananchi watapata fursa ya kujua NGOs wanafanya nini na pia limetengwa dirisha maalum kwa ajili ya wadau kutoa taarifa kwa Msajili wa NGOs kuhusu utendaji kazi wa NGOs. Swali 4: Je, Kuna uwezekano wa kupata Cheti cha Ukubalifu na kile cha Usajili katika ngazi ya Mkoa na Wilaya? Jibu: Kwa sasa utaratibu wa kutoa vyeti vya Usajili na Ukubalifu unafanyika tu katika Ofisi ya Msajili wa NGOs Makao Makuu ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dar es Salaam. Hii ni kuhakikisha kwamba kunakuwepo udhibiti katika utoaji wa vyeti ili kuzuia vitendo vya udanganyifu. Utoaji wa vyeti kwa ngazi tofauti unaweza kufanyika pale tu tutakapokuwa tumeweza kuunganisha benki ya takwimu kupitia mawasiliano ya mtandao kwa njia ya kompyuta kwa ngazi zote. Swali 5: Wafadhili wanapokuja nchini, wenyeji ni Serikali. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuwaunganisha na NGOs? Jibu: Kimsingi wafadhili wa shughuli za NGOs wanapokuja nchini hawapitii Serikalini kwani hupendelea kuwasiliana na NGOs zenyewe moja kwa moja. Aidha, inapotekea baadhi yao kupitia Serikalini inakuwa sio rahisi kwa Serikali kuwasiliana na NGO moja moja. Kwa kuwa sasa kuna chombo cha kitaifa cha NGOs yaani Baraza la Taifa la NGOs mawasiliano yote yatapitia huko. Serikali inaamini kuwa ni jukumu la Baraza la Taifa la NGOs kuunganisha NGOs na Wafadhili. Swali 6: Kanuni za Maadili za NGOs, zimetangazwa katika Gazeti la Serikali namba ngapi? Jibu: Kanuni za Maadili ya NGOs zilitangazwa katika Gazeti la Serikali, Toleo Na. 363 la tarehe 5 Desemba, 2008. Swali 7: Shirika likiwa limesajiliwa chini ya Sheria ya Vyama, Wizara ya Mambo ya Ndani hivyo mali itakayokuwanazo sio mali za shirika?. Je, lisajiliwe upya? Jibu: Sheria ya NGOs Na. 24 ya mwaka 2002 inatoa fursa kwa asasi zilizosajiliwa chini ya Sheria ya Vyama kupata Cheti cha Ukubalifu ambacho kina hadhi au sifa sawa na usajili wa kawaida wa NGO. Mahitaji ya usajili ni haya yafuatayo:- (i) Katiba 3 zilizojaladiwa. (ii) Nakala 2 za muhtasari kwa ajili ya kupata compliance. (iii) Wasifu wa viongozi (CV) yaani (Mwenyekiti, Katibu na Mweka Hazina) na picha zao mbili mbili kwa kila CV. (iv) Fomu ya maombi ya NGO Na. 3. (v) Barua ya maombi na nakala ya cheti viambatanishwe. (vi) Barua ya Msajili Msaidizi kwenye ngazi husika. Usajili chini ya Sheria ya NGOs Na. 24/2002 unatoa fursa kisheria kwa shirika husika kumiliki mali hivyo shirika ambalo limesajili chini ya Sheria ya Vyama na kupata Cheti cha Ukubalifu basi wanapata hadhi ya kumiliki mali. Swali 8: Mbinu zipi zifanyike ili wadau wa sekta ya NGOs wapate Sheria ya Mashirika hayo? Jibu: Idara ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali inayo Tovuti ambayo inaweza kutumika kupata sio tu Sheria, bali pia nyaraka zote muhimu kama fomu za usajili, Sera ya Taifa ya NGOs, Fomu Na. 10 ya kutuma taarifa ya kazi ya mwaka, Kanuni za Maadili ya NGOs, na hata dirisha la kutoa taarifa kuhusu utendaji wa NGOs kwenye maeneo yenu. Anuani ya Tovuti hii ni www.tnnc.go.tz Wadau wote wanahimizwa kutumia Tovuti hii kikamilifu ili kurahisisha utendji wao wa kazi na kuongeza uwazi na uwajibikaji. Swali 9: Je, ni Asasi zipi zinazosajiliwa Mambo ya Ndani na zipi zinazosajiliwa na Sheria ya NGOs? Jibu: Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto inasajili Mashirika yanayohudumia jamii tu kwa ujumla, maarufu kama NGOs. NGOs hizo huwa na sifa mbalimbali kama vile; mfumo wa kufanya mikutano, huainisha kwa kina inafanyaje shughuli zake; huwa na mfumo na mawasiliano unaoaminika na kuwa na uongozi unaoonesha namna gani kiongozi anapatikana/kuingia madarakani na taratibu za uwajibikaji kwa njia ya vikao. Wizara ya Mambo ya Ndani kwa mujibu wa Sheria ya Vyama haisajili NGOs bali Vyama. Vyama hivi ni pamoja na Mashirika au Taasisi za kidini, Klabu za burudani zinazohudumia wanachama tu au vyama vya kusaidiana wakati wa shida na raha. Hata hivyo Mashirika ambayo yako chini ya Taasisi za dini lakini yanatoa huduma kwa jamii bila kujali imani au itikadi ya kidini yanaweza kusajiliwa chini ya Sheria ya NGOs, mfano CARITAS. Swali 10: Je, taratibu za kusajili CBOs ni zipi? Jibu: Kwa kawaida CBOs hufanya kazi katika ngazi za mtaa na mara nyingi huwa hazisajiliwi, bali hupewa utambulisho maalum kutoka kwa mamlaka husika inakofanyia kazi. Hata hivyo, iwapo CBO ina dira na malengo ya kufanya kazi katika wilaya nzima, basi inaweza kusajiliwa katika ngazi tajwa chini ya Sheria ya NGOs kwa kuwa sasa sifa yake inakuwa imebadilika kutokana na upeo wa kuendesha shughuli zake. Swali 11: Je, Wajibu wa mitandao ya NGOs ni upi? Jibu: Lengo kuu la mitandao ya NGOs yote nchini, ni kuzijengea uwezo na kuziwezesha NGOs kujitegemea na kubwa zaidi ni kujiendesha zenyewe bila ya kuwa tegemezi kwa wafadhili. Hivyo basi, mafunzo mbalimbali ya uongozi, mawasiliano, maadili, uwajibikaji yamekuwa yakitolewa na mitandao hiyo ili kufikia malengo yake. Kimsingi mitandao ya jinsi hii huanzishwa kwa kuzingatia na kutegemea mahitaji ya wadau kwenye eneo husika na si vinginevyo. Uzoefu umeonesha kuwa mitandao ambayo huanzishwa kwa kutumia utaratibu huu imekuwa na mafaniko makubwa kwa kuwa inayo mizizi ambayo inakidhi haja na matakwa ya wadau katika maeneo yao ya kazi. Aidha, Baraza la Taifa la NGOs limekuwa likishirikiana bega kwa bega na mitandao ya NGOs katika ngazi zote. Kwa mantiki hii, mitandao ni kiungo bora na mahsusi kwa utendaji mzuri wa Baraza hili. Aidha, kupitia mitandao ya NGOs, jambo lolote likizungumzwa (addressed), Serikali husikiliza haraka na ukaribu zaidi kuliko NGO moja moja kuzungumza peke yake/zenyewe kwa kuwa inawakilisha sauti na matakwa ya wengi. Swali 12: Baraza la Taifa la NGOs ni la Kitaifa. Je, hakuna Baraza la kiwilaya na kimkoa? Kwa njia hiyo kuna maendeleo yatafikiwa kweli? Jibu: Baraza la Taifa la NGOs liko ngazi ya Taifa na kimuundo haliko katika ngazi ya kiwilaya na kimkoa. Aidha, katika uendeshaji shughuli zake hutumia mitandao ya NGOs ya Kimikoa na Kiwilaya. Kwa njia hii wadau wanapata fursa nzuri ya kushiriki katika maamuzi mbalimbali kwa kuwa mitandao hii ipo Tanzania nzima. Swali 13: Mwanasheria toka Wizara ya Mambo ya Ndani, alikuja kuhamasisha usajili kupitia Sheria yao ya Vyama mkoani Shinyanga. Alieleza kuwa waliosajiliwa chini ya Sheria ya NGO hukosa kutambulika nje ya nchi, na hivyo kupelekea kukosa ufadhili wa nje. Je, hivyo ni sahihi? Jibu: Huo ni udanganyifu, kwani Mashirika yaliyosajili chini ya Sheria ya NGOs Na. 24 ya mwaka 2002, hutambulika Kisheria ndani na nje ya nchi. Hata hivyo, uzoefu unaonesha wazi kuwa Wafadhili wengi wamekuwa wakija kwa Msajili wa NGOs kuthibitishwa uhalali wa usajili wa Mashirika mengine ambayo yamesajiliwa chini ya Sheria nyingine kama ni NGO au la. Ndio maana Sheria ya NGOs inatoa fursa kwa Mashirika yaliyosajiliwa kwa mujibu wa Sheria nyingine ikiwamo Sheria ya Vyama na ambayo yana hadhi na sifa ya kuwa NGOs kuomba Cheti cha Ukubalifu ili watambulike kama NGOs. Swali 14: Je, shirika linasajiliwa kwa kikundi tu, au hata mtu mmoja mmoja? Jibu: Kwa mujibu wa Sheria ya NGOs usajili hautolewi kwa mtu mmoja mmoja au wawili. Kimsingi usajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, hufanyika/hutolewa kwa watu walio katika kikundi kuanzia 5 au zaidi. Swali 15: NGO iliyosajiliwa Ofisi ya Makamu wa Rais, kuna utaratibu wa kulipa ada ya mwaka ambayo ni shs. 50,000/=. Kwa sasa utaratibu wa kulipia ada hiyo ukoje? Jibu: Ni kweli kuanzia mwaka 1996 hadi Januari, 2006 Idara ya Uratibu wa NGOs ilikuwa chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais. Hata hivyo, katika Serikali ya Awamu ya Nne, Makamu wa Rais alipunguziwa majukumu na hivyo kuanzia mwezi Februari 2006, jukumu la kuratibu NGOs lilihamishiwa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto. Aidha, wakati huo ada ya Usajili wa NGOs ilikuwa ikilipiwa mikoani kupitia Ofisi za Hazina Ndogo (Sub-Treasury). Kufuatia usumbufu mkubwa uliojitokeza kwa wadau kupitia njia hii, iliamuliwa kusitishwa na hivyo kulipwa moja kwa moja Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto. Kwa sasa njia ya haraka inayotumika ni kwa watu kuungana na kumtuma mwakilishi mmoja Makao Makuu ya Wizara (DSM) ili kulipia ada na stakabadhi za malipo husika hutolewa. Swali 16: Je, Wajumbe wa Baraza ya Taifa ya Uratibu wa NGOs hudumu kwa muda gani? Jibu: Kwa mujibu wa Sheria ya NGOs Na. 24 ya mwaka 2002, kifungu Na. 26 (a) Wajumbe wa Baraza la Taifa la NGOs hudumu kwa muda wa miaka mitatu (3) tu na wanaweza kuchaguliwa tena kwa kipindi kisichozidi miaka 3. Swali 17: Kuna uhusiano gani kati ya NGOs na Serikali za Mitaa? Jibu: Serikali na NGOs ni wabia muhimu katika maendeleo. Ubia huu umejikita hasa katika kuhakikisha kuwa pande zote mbili zinafahamu malengo na taratibu za utendaji kazi katika maeneo mbalimbali kulingana na mpango wa kazi. Ni vizuri NGOs zikaingiza mipango yao kwenye mipango ya Halmashauri ili kuepuka ‘dublication’ katika utoaji wa huduma. Aidha, Halmashauri zinaweza kuzipa NGOs fedha kwa ajili ya kutekeleza majukumu yao (outsourcing) iwapo watatambua na kuhuisha mipango yao pamoja. Hata hivyo, Bodi inayahimiza Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kuboresha mahusiano yao miongoni mwa wanachama na kuongeza uwazi katika kutoa taarifa zao. Swali 18: Kwa kuwa viongozi wa NGOs hawashitakiwi binafsi kwa makosa ya NGOs zao, je, ni nani anazitetea NGOs pindi zinaposhitakiwa? Ni Serikali? Jibu: Kutoshitakiwa kwa viongozi wa NGOs pindi shirika linapofanya kosa hakumaanishi kuwa watatetewa na Serikali bali, linaloshitakiwa ni shirika. Kwa kuwa viongozi hao ni sehemu ya shirika basi watahusika kama shirika na siyo wao binafsi. Serikali haiwezi kuzitetea taasisi hizi mahakamani kwa kuwa NGOs ni vyombo huru ambavyo kwa mujibu wa Sheria hii, NGOs zinaweza kushitaki au kushitakiwa. Swali 19: Kwa kuwa, NGOs ni mdau wa Serikali, Je ina maana kuwa wanafanya kazi kwa niaba ya Serikali au Wananchi? Jibu: Kimsingi NGOs si mbadala na wala hazifanyi kazi kwa niaba ya Serikali bali hutoa huduma mbalimbali kulingana na matakwa au matatizo ya sehemu husika. Hii inatokana na ukweli kuwa Serikali na NGOs wanao uwezo tofauti katika kutekeleza majukumu yao ya kimsingi. Kuna mambo ambayo NGOs zina uwezo mzuri kuliko Serikali na kuna maeneo mengine Serikali ina uwezo kuliko NGOs. Hivyo wote wanashirikiana na kuunganisha nguvu zao katika kuhudumia wananchi. Udau au Ubia tunaozungumzia ni katika nyanja za kufanya kazi au kutoa huduma kulingana na uwezo wa kutenda jambo fulani (comparative advantage). Swali 20: Je, ni wakati gani NGOs zinaweza kuomba ruzuku kutoka Serikalini? Jibu: Hakuna utaratibu maalum wa Serikali kutoa ruzuku kwa NGOs kwa kuwa ufuatiliaji wa Shirika moja moja ni mgumu na usiokuwa na tija. Hata hivyo, wakati ukifika Serikali inaweza kutoa fedha kwa Baraza la Taifa la NGOs kwa ajili kutoa ruzuku kwa NGOs kwani ni chombo chenu na tayari kimeweka maadili kwa ajili ya NGOs kujithibiti wenyewe. Chombo hiki kinatakiwa kuweka mifumo ya ndani ya kifedha na taratibu za uendeshaji shughuli zao itakayohakikisha kunakuwepo na uwajibikaji ulio wazi. Aidha, ni vema kianzishe taratibu za NGOs zenyewe kujifanyia tathmini yao wenyewe kwa kuzingatia kanuni za maadili ya NGOs na vigezo vingine vitakavyowekwa na sekta yenyewe. Utaratibu huu utasaidia kuondoa ubabaishaji na kuimarisha utendaji wa sekta ya NGOs nchini. Swali 21: Je, NGO ni nini? Inatofautishwaje na Vyama vya Wafanyakazi na Vikundi vya Kijamii (CBOs)? Jibu: Kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya NGOs, “Shirika Lisilo la Kiserikali ni kikundi binafsi na cha hiari cha watu au mashirika ambayo ni huru na si kwa ajili ya kugawana faida ambacho kimeundwa katika ngazi ya jamii, kitaifa na kimataifa kwa lengo la kukuza maendeleo halali ya kiuchumi, kijamii au kiutamaduni au kushawishi au kutetea juu ya hoja zenye maslahi kwa umma au maslahi ya kikundi cha watu au mashirika” Kimsingi NGOs ni mashirika yenye sifa zifuatazo: (i) Hulenga kusaidia jamii; (ii) Wanachama wake hujiunga kwa hiari; (iii) Yana muundo unaotambulika kisheria; na (iv) Wanachama wake hawalengi kugawana faida. Vikundi vya Kijamii (CBOs) mara nyingi havisajiliwi kisheria na hufanya kazi katika ngazi ya kijiji, kata au mtaa na malengo yake makubwa ni kusaidiana wao kwa wao tu. Vyama vya Wafanyakazi hulenga kusaidia na kutetea maslahi ya wafanyakazi walioajiriwa na Serikali au Taasisi Binafsi ambao ni wanachama wake tu. Swali 22: Je, kuna tofauti gani kati ya Msajili na Wasajili Wasaidizi wa ngazi ya Wilaya na Mkoa? Jibu: Kwa mujibu wa Sheria ya NGOs, Wasajili Wasaidizi wa NGOs huteuliwa na Msajili Mkuu wa NGOs ili kusaidia kushughulikia na kuwezesha usajili wa mashirika haya katika ngazi ya Wilaya na Mkoa. Aidha, Wasajili Wasaidizi ni waratibu na wafuatiliaji wa shughuli za NGOs katika maeneo yao, hivyo hutakiwa kutoa taarifa kwa Msajili Mkuu wa NGOs. Kwa NGOs ambazo hufanya kazi katika ngazi ya Taifa na Kimataifa usajili wao hufanyika moja kwa moja kwa Msajili Mkuu wa NGOs pasipo kupitia kwa Wasajili Wasaidizi. Aidha, maombi ya usajili wa NGOs katika ngazi ya Wilaya na Mkoa hushughulikiwa na Wasajili Wasaidizi na Msajili hupokea maombi hayo na kutoa Cheti cha Usajili/Ukubalifu kwa ngazi ya Wilaya na Mkoa. Swali 23: Sera ya Taifa ya NGOs inapatikanaje? Jibu: Sera yaTaifa ya NGOs inapatikana kwenye Tovuti ya Idara ya Usajili na Uratibu wa NGOs nchini kwa anuani ya www.tnnc.go.tz. Wote mnahimizwa kuisoma na kuielewa vizuri maana ndio mwongozo wetu mkuu wa utendaji na uendeshaji wa shughuli za NGOs nchini. Aidha, ni jambo la busara kwa wale wenye uwezo baada ya kupata sera hii kuisambaza kwa wadau na wanachama wenu ili kuwa na uelewa wa pamoja mnapotekeleza majukumu yenu. Kutokana na uzoefu wenu kulingana na matokeo ya utendaji kazi wenu pamoja na changamoto mnazozipata kwenye sekta itakuwa pia fursa muafaka kwa wadau kutoa maoni yatakayosaidia kuboresha Sera hii wakati wa kuifanyia mapitio. Swali 24: Baraza linatambua makundi maalum na hasa walemavu? Je, walemavu si kundi maalum? Jibu: Watu wenye ulemavu ni muhimu sana katika maendeleo ya Taifa. Kimsingi Baraza la Taifa la NGOs linatambua na kutoa kipaumbele kwa watu wenye ulemavu. Katika kutekeleza hilo Baraza limetenga nafasi 2 za wajumbe wa Baraza kuwakilisha maslahi ya watu wenye ulemavu ambao hupatikana kwa njia ya kuchaguliwa na wadau wa NGOs zinazoshughulikia masuala ya watu wenye ulemavu. Swali 25: Je, Kuna tofauti ipi kati ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs), Asasi za Kiraia (CSOs) na Vikundi vya Kijamii (CBOs) Jibu: Katika tafsiri pana NGOs na CBOs zote ni sehemu ya Asasi za Kiraia (CSOs), lakini si kila CSO ni NGO katika maana kuwa NGOs ni kundi dogo katika jamii ya CSOs. NGOs husajiliwa wakati CBOs kwa upande wake, hazina usajili popote mbali ya kutambuliwa na Halmashauri mahali zinapofanya kazi zake, hasa katika ngazi ya mtaa, kijiji au kata. NGOs hutoa huduma kwa jamii katika ujumla wake wakati CBOs mara nyingi zinalenga kusaidia wananchama tu katika ngazi husika. Swali 26: Je, kuna tofauti gani kati ya Usajili chini ya Sheria ya NGOs na Sheria ya Vyama. Jibu: Usajili wa Vyama hufanywa kwa mujibu wa Sheria ya Vyama, Sura 337 wakati Usajili wa NGOs hufanywa kwa mujibu wa Sheria ya NGOs Na. 24 ya mwaka 2002 kama ilivyorekebishwa mwaka 2005. Sheria ya Vyama inasajili vikundi mbalimbali ambavyo si NGOs kama vile vikundi vya dini, vyama vya kusaidiana, vyama vya wafanyakazi, vikundi vya starehe, n.k. Vikundi ambavyo vina sifa ya kuwa NGOs ambavyo vimesajili chini ya Sheria ya Vyama vinapaswa kwa mujibu wa Sheria ya NGOs kuomba na kupatiwa Cheti cha Ukubalifu. Sheria ya NGOs inasajili Mashirika yenye sifa ya NGOs kama ilivyooneshwa kwenye Swali Na. 21 na si vinginevyo. Swali 27: Serikali imechukua hatua zipi katika kuzijengea uwezo NGOs, hususan katika uandishi wa “miradi” na uwiano uliopo kati ya mashirika yanayofanya kazi mijini na vijijini? Jibu: Kimsingi Serikali haina utaratibu wa kusaidia NGOs katika uandishi wa miradi kwa lengo la kupata fedha za kuendesha shughuli zao. Aidha, suala hili lina ugumu wake kwa vile kila mfadhili ana vigezo na taratibu anazozingatia katika kutoa fedha kulingana na masharti waliyojiwekea. Kutokana na uzoefu tulionao taasisi kama vile FCS, Mitandao ya Kitaifa, Kimkoa na Kiwilaya wamekuwa wakizijengea uwezo NGOs ikiwezo na uandishi wa miradi na ubunifu. Hata hivyo, wadau wa Sekta ya NGOs wanahimizwa kujenga tabia ya kutafuta fedha kutoka vyanzo vya ndani badala ya kutegemea wafadhili wa nje ambao pindi wakikatiza misaada shirika haliwezi kuendelea na pengine kufa kabisa. Ni vema kwa NGOs kutambua kuwa kinachozuiliwa ni kugawana faida au mali na si kutengeneza faida. Faida katika NGOs ni muhimu sana ili itumike kuendeleza malengo ya asasi, hivyo NGOs zinahimizwa kuwa wabunifu na kuanzisha miradi mbalimbali itakayosaidia kuwajengea uwezo kifedha. Baadhi ya NGOs ambazo zimejijengea uwezo wa kutafuta fedha wao wenyewe ni Hakikazi Catalyst ya Arusha, TAGRODE ya Iringa, KADETFU ya Kagera, n.k. Bodi inaamini kuwa mitandao ya NGOs ya Kitaifa na Kimkoa imekuwa ikifanya kazi hiyo ya kuwajengea uwezo NGOs katika maeneo yenu. Katika suala hili ni vema Baraza la Taifa la NGOs na Mitandao ya Kitaifa na Kimkoa kuunganisha nguvu ili tuweze kupata matokeo mazuri na ya kuridhisha. Swali 28: Bodi inashauri nini kuhusu suala la NGOs kutapakaa zaidi maeneo ya mijini kuliko vijijini? Jibu: NGO ni chombo huru kinachoanzishwa na wanachama kwa hiari yao hivyo si rahisi kwa Bodi kuzichagulia NGOs maeneo ya kufanyia kazi. Bodi inaamini kuwa wadau wa Sekta ya NGOs wanafahamu umuhimu wa kuwa karibu na wananchi wanakotoa huduma kuliko kukaa mijini tu. Suala hili litaweza kutekelezeka vizuri zaidi na NGOs wenyewe kupitia Kanuni za Maadili ya NGOs ambazo zinalenga kujenga na kuinua taswira ya sekta ya NGOs nchini. Hata hivyo Bodi inawahimiza wadau wa Sekta ya NGOs nchini kutandaa katika maeneo ya vijijini ili kuleta ufanisi katika utendaji kazi na kuwaletea wananchi maendeleo. Ni jambo la kutambua kuwa wananchi wote Tanzania wanayo haki ya kupatiwa huduma bila ubaguzi kwa misingi ya maeneo walipo iwe mijini au vijijini kwa kuwa NGOs hutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia dira na madhumuni ya kuanzishwa kwao. Swali 29: Je, muundo wa Bodi ukoje, ina idadi gani ya wajumbe na madhumuni yake yapi? Jibu Kwa mujibu wa Sheria ya NGOs Na. 24 ya mwaka 2002, kwenye jedwali chini ya kifungu cha 7(2) Bodi inaundwa na wajumbe 10. Kati ya hawa wajumbe wanne (4) kutoka sekta ya NGOs wanateuliwa na Waziri mwenye dhamana ya uratibu wa NGOs kwa mapendekezo ya Baraza la Taifa la NGOs na wajumbe watano (5) wenye uzoefu na uelewa wa masuala ya sekta ya NGOs huteuliwa na Waziri mwenye dhamana ya uratibu wa NGOs kama wawakilishi wa Serikali na mjumbe mmoja (1) ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi huteuliwa na Rais. Aidha, wajumbe watano wanaoteuliwa na Serikali wanaweza hata kutoka kwenye sekta ya NGOs hivyo si lazima wawe Serikalini. Kwa mfano kwa sasa Bodi inayomaliza kipindi chake ina mjumbe amabye ameteuliwa na Serikali lakini ametoka kwenye sekta ya NGOs. Swali 30: Majukumu ya Ofisa Tawala wa Wilaya na mipaka yao katika usajili ni ipi? Jibu: Afisa Tawala ni mwakilishi wa Msajili wa NGOs katika ngazi ya Wilaya, hivyo ni Msajili Msaidizi katika ngazi hiyo. Majukumu yake ni kushughulikia hatua za awali kama kupokea maombi rasmi ya usajili kwa mashirika yenye nia ya kufanya kazi katika ngazi ya Mkoa na Wilaya. Baada ya kupitia maombi hayo huwasilishwa kwa Ofisi ya Msajili wa NGOs, Dar es Salaam. Kiutendaji cheti cha Usajili hutolewa kwenye Ofisi ya Msajili Makao Makuu na sio kwa Wasajili wasaidizi. Swali 31: Je, Maofisa Tawala na Maofisa Mipango wa Wilaya ambao ni Wasajili Wasaidizi wa NGOs wamejengewa uwezo katika mchakato wa Usajili? Jibu: Wasajili Wasaidizi wa NGOs ni viungo muhimu katika kurahisisha usajili wa NGOs chini ya Sheria ya NGOs Na. 24 ya mwaka 2002. Mara tu baada ya kupitishwa kwa Sheria hii mwaka 2002 na kuanza kufanya kazi rasmi mwaka 2005, Wasajili Wasaidizi walipatiwa mafunzo rasmi na kupewa weledi juu ya Sera ya Taifa ya NGOs, Sheria ya NGOs na taratibu za usajili ndipo waliteuliwa rasmi kuwa Wasajili Wasaidizi. Kimsingi wanaouelewa mpana kuhusu taratibu hizo na kwa kweli wamekuwa wakifanya kazi nzuri. Changamoto iliyopo ni kwenye maeneo ambayo wale waliopewa mafunzo wamestaafu, wakaajiriwa watumishi wengine wapya na baadaye kuteuliwa kushika nyadhifa hizo. Hata hivyo, utaratibu wa kuwateua Maafisa Maendeleo ya Jamii kuwa Wasajili Wasaidizi umekamilika kwa kuwa kiutendaji wao ndio wanashughulikia NGOs. Swali 32: Nini mtazamo wa Serikali kwa NGOs hasa zile zinazofanya kazi za utetezi na ushawishi kama ilivyo Haki Elimu? Jibu Serikali na NGOs ni wabia muhimu katika maendeleo. Serikali inatambua umuhimu wa wadau hawa na kuthamini mchango wao kitaifa ndio maana imezipatia NGOs za namna hii usajili ili ziweze kutekeleza shughuli zao kihalali. Ni vema kutambua kuwa Serikali haizuii mashirika haya kufanya kazi za ushawishi na utetezi isipokuwa katika utendaji kazi wao yanatakiwa kuheshimu haki, taratibu na misingi ya utawala bora. Swali 33: Je, muundo wa Baraza la NGOs ni ukoje? Jibu: Kwa mujibu wa kifungu cha 25(3) cha Sheria ya NGOs Na. 24 ya mwaka 2002, Baraza la Taifa la NGOs lina wajumbe 30 ambao hukaa madarakani kwa kipindi cha miaka mitatu kutoka maeneo yafuatayo:-  Wawakilishi wa mikoa………………………………………………………….. 21  Wawakilishi wa mitandao ya kitaifa (TANGO &TACOSODE)…..... 2  Mitandao ya makundi maalumu - ukeketaji, UKIMWI…….…......... 2  Mitandao ya Kimkoa ……………………………………………………………... 2  Wawakilishi watu wenye ulemavu……….……….……………………….. 2  Mwakilishi NGOs za kimataifa……………………………………………….. 1 Swali 34: Kuna uhusiano gani kati ya Bodi na Baraza? Jibu: Baraza la Taifa la NGOs na Bodi ya Taifa ya Uratibu wa NGOs ni vyombo vya kitaifa vilivyoundwa kwa mujibu wa Sheria ya NGOs Na. 24 ya mwaka 2002. Baraza la Taifa la NGOs limeundwa ili kuwezesha Sekta ya NGOs kujitawala kupitia Kanuni za Maadili ya NGOs. Aidha, Baraza hili ni sauti ya sekta ya NGOs nchini katika kutetea maslahi ya sekta hii. Vyombo hivi viwili vimejikita katika kuhakikisha kuwa mazingira mazuri kwa NGOs kutekeleza majukumu yao yanakuwepo. Kutokana na mahusiano hayo, wajumbe wanne (4) kutoka Baraza la Taifa la NGOs wanateuliwa na Waziri mwenye dhamana ya uratibu wa NGOs kuwa wajumbe wa Bodi ya Taifa ya Uratibu wa NGOs. Wajumbe hawa hutoa mrejesho kwa Bodi kuhusu masuala ya Sekta ya NGOs na kiungo muhimu kati ya Bodi na Baraza. Swali 35: Kuna uhusiano gani kati ya “the Foundation for Civil Society” na Bodi/Baraza? Jibu: The Foundation for Civil Society (FCS) ni Taasisi ya kiraia kama zilivyo NGOs nyingine, tofauti ni kuwa Shirika hili hutoa fedha kwa ajili ya kuzijengea uwezo NGOs nchini na kukuza ushindani miongoni mwa wadau wa sekta hii. Taasisi hii hutoa fedha kwa NGOs kwa ajili ya kuendesha miradi mbalimbali, kujengea uwezo NGOs na wananchi, usajili na utawala bora. Bodi haipati fedha yoyote kutoka FCS kwa ajili ya kujiendesha katika shughuli zake. Aidha, Bodi imeanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya NGOs Na. 24 ya mwaka 2002 wakati FCS imesajiliwa chini ya Sheria ya Makampuni. Baraza la Taifa la NGOs nalo limeanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya NGOs kwa lengo la sekta ya NGOs kuwa na chombo chao kikuu cha kujisimamia kupitita utekelezaji wa Kanuni za Maadili. Aidha, chombo hiki kinaweza pia kupata fedha kutoka FCS na wafadhili wengine. Swali 36: Bodi inaweza kusaidia FBOs kupata ruzuku ya Foundation? Jibu: Kimsingi FBOs zinaweza kusajiliwa chini ya Sheria ya NGOs Na. 24 ya mwaka 2002 ili mradi malengo yake si kuhubiri dini bali kutoa huduma kwa jamii nzima kwa ujumla. Aidha, FBOs wanaweza kupata ruzuku kama NGOs nyingine. Hata hivyo, Bodi haiwezi kuingilia utaratibu ambao ‘the Foundation’ wamejiwekea katika kutoa ruzuku hiyo. Uamuzi wa nani apate na nani asipate ruzuku unabaki kuwa ni wa Shirika lenyewe kulingana na vigezo walivyojiwekea. Bodi inapenda kuzishauri FBOs kama wadau wengine wa Asasi za Kiraia kupeleka maombi yao ya ruzuku kwa FCS. Swali 37: Sheria ya NGOs inasemaje kuhusu wanachama waanzilishi waliomaliza muda wao katika nyadhifa zao kuendelea kutumika katika Mashirika yao ili waweze kuwa hazina ya Taifa? Jibu: Suala la wanachama waanzilishi waliomaliza muda wao katika nyadhifa mbalimbali kutumiwa na Shirika liko mikononi mwa wanachama wenyewe chini ya kanuni na taratibu walizojiwekea. Hata hivyo, kwa kuwa NGOs ni mashirika huru yanayojiendesha yenyewe, kisheria Serikali haiwezi kuingilia. Jambo la msingi ni kwamba uamuzi wowote wa kuwatumia wanachama waanzilishi sharti ukubaliwe na wanachama wote kwenye mkutano mkuu ili kuondoa migogoro inayoweza kujitokeza kutokana na baadhi yao kutoridhika. Swali 38: Bodi inafuatiliaje Taasisi za Kimataifa ambazo ziko hapa nchini na zinafanya mambo yasiyokubalika? Jibu: NGOs za kimataifa zinapoingia Nchini kufanya kazi husajiliwa kwanza na kupata Cheti cha Usajili kama NGOs nyingine. Aidha, hutakiwa kuingia mkataba na Serikali ambao unaainisha majukumu yao wakati wakiwa hapa nchini ili kufanya kazi kwa misingi ya Sheria zilizopo. Hata hivyo, Bodi huwa haiingilii taratibu za nani apewe fedha na Mashirika haya na nani asipewe. Kimsingi Bodi inalichukulia suala hili kuwa changamoto na itakuwa vema Bodi, Baraza na wadau washirikiane kutatua tatizo hili kwa kuwa mashirika haya pia wanaye mwakilishi wao kwenye Baraza la Taifa la NGOs. Swali 39: Watumishi wa NGOs wanahitaji kupata msamaha wa kodi ili kununua vifaa ikiwemo magari kutoka nje. Je, Bodi inaweza kusaidia kuhusu suala hili hasa ikizingatiwa kuwa mishahara ya watumishi hao inalingana na ya wenzao walioko Serikalini? Jibu: Watumishi wa Serikali wanapoagiza vitu kutoka nje ya nchi hupata kodi ya ongezeko la thamani (VAT) na kusamehewa ushuru wa forodha (custom duty) ikiwa ni msamaha wa kodi kwa sehemu tu na sio wote. Hii ina maana nusu ya gharama hizo huchangiwa na mtumishi mwenyewe. Hata hivyo, Bodi inawashauri wadau wa sekta ya NGOs kupitia kwenye Baraza lao la Taifa la NGOs kufuatilia suala hili Mamlaka ya Mapato Tanzania. Suala hili litakuwa na uzito iwapo litapelekwa na Baraza la Taifa la NGOs kwa kuwa ni jukumu lao halafu Bodi itaombwa ushauri tu na Mamlaka ya Mapato Tanzania. Swali 40: Je, Ni kwa namna gani NGOs zilihusishwa katika kutengeneza Kanuni za Maadili yao? Jibu: Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali lilishirikisha NGOs kwa kiasi kikubwa katika kutengeneza Kanuni za Maadili ya NGOs kwa kuzisambaza katika mikoa yote ya Tanzania Bara ili kupata maoni yao. Aidha, mitandao yote ya Kimkoa na Kiwilaya ilishirikishwa kikamilifu kwa njia ya mikutano na wengine walichangia kupitia njia ya mtandao. Hata hivyo, kuna kipengere kinachotoa fursa kwa NGOs kuzifanyia marekebisho kanuni hizo pale inapobidi. Swali 41: Je, Kuna hoja ya NGOs kutaka uwakilishi Bungeni? Jibu: Wadau wa Sekta ya NGOs waliwasilisha kwa Spika wa Bunge barua inayotaka kuwepo na utaratibu maalum wa kuteua mwakilishi wa NGOs Bungeni bila kupitia Vyama vya Siasa. Kuhusu kuwepo kwa mwakilishi wa NGOs Bungeni kupitia Chama Cha Mapinduzi ni utaratibu wa chama hicho na si utaratibu wa Bunge. Suala hili ni vema lifanyiwe kazi na NGOs wenyewe na tunaamini FCS kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la NGOs wamekutana na wabunge na hoja hiyo kuzungumziwa kwa kina. Ni muda muafaka sasa kwa NGOs kupitia vyombo vyenu kufuatilia suala hili kikamilifu.  
  Source:  
     
  :: Home :: About Us :: NGO Profiles :: Site Map :: Feedback :: Contact Us